MGOMBEA ubunge wa jimbo la Kahama, James Lembeli kupitia tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ameishambulia serikali ya CCM na kueleza kwamba serikali hiyo haiwezi kuwapatia wananchi maendeleo kutokana na kuwa na mfumo mbovu wa kiutawala.
Mbali
na hilo Lembeli alisema serikali ya CCM ndiyo serikali pekee yenye
mfumo kandamizi, viongozi wake ni walaghai wakubwa na imekuwa na mfumo
mchafu wa kulindana mafisadi kwa mafisadi huku wananchi wa kawaida
wakiendelea kutaabika.
Lembeli
ambaye awali alikuwa mbunge wa CCM jimbo la Kahama na baadaye kutimkia
Chadema, alitoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa kampeni za Chadema
zilizofanyika katika viwanja vya Freeman Mbowe ambapo uwanja huo
ulijengwa na mbunge anayemaliza muda wake na kutetea jimbo hilo Prof
Kulikoyela Kahigi.
Kiongozi
huyo ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa kampeni hizo
alitonesha vidonda vya wafugaji wa jimbo hilo kwa kueleza kwamba
serikali imekalia ripoti ya uchunguzi wa Tume iliyoundwa na bunge kwa
ajili ya Operesheni tokomeza.
Alisema
sababu kubwa ya serikali kushindwa kuweka hadharani taarifa hiyo ambayo
Lembeli alikuwa mwenyekiti ni kutokana na vitendo vingi vilivyofanywa
vilikuwa vikihusisha vigogo wa serikali na ndiyo maana kuna hali ya
kulindana licha ya kuwa wapo watu ambao wamepata vilema na wengine
kupoteza maisha.
Alisema
katika taarifa hiyo kuna mambo mengi ya kutisha ambayo yalifanywa na
watumishi wa serikali ikiwa ni pamoja na kudhalilisha utu wa mtu, mauaji
pamoja na uharibifu wa mali za wananchi hususan wafugaji.
“Ndugu
zangu wana Bukombe kuna msemo usemao siri ya mtungi aijuaye kata, sasa
mtungi ni CCM na kata ni mimi (Lembeli) mimi nimetoka CCM baada ya kuona
kwamba hakuna chama dharimu, kandamizaji, kinachotumia migogo ya
wanyonge masikini kujinufaisha.
“Sijaona
chama chenye viongozi ambao wanalinda ufisadi wa kutisha, wizi wa
kutisha pamoja na watu ambao hata upeo wa kufikiri umekwisha bali
wamekuwa watu wa kupokea vitisho vya hali ya juu na hatima yake
wanatugeuza kuwa wapumbavu na malofa,” amesema Lembeli.
Akizungumzia
ahadi za mgombea urais kupitia CCM, Dk. John Magufuli, Lembeli amesema
kwamba mgombea huyo kwa sasa amekuwa akiwalaghai wasukuma kwa madai
kwamba atawapatia maendeleo pale tu atakapochaguliwa.
Amesema kauli hiyo ni ya uongo na unafiki kamwe Dk. Magufuli awezi hata kuwatetea wasukuma wenzake.
“Nawapa
mifano miwili tu wakati Dk. Magufuli akiwa waziri wa mafugo aliwasaidia
nini wafugaji wakati mifugo ikiteketea na kukosekana kwa soko.
“Mbali
na hilo alipochaguliwa kuwa waziri wa mifugo na uvuvi ni nani ambaye
alikuwa akichoma kokolo za wavuvi kwa madai hazifahi, alikuwa wapi
kushika nyavu hizo zikiwa madukani na kuzipiga marufuku wakati huo huo
aliendelea kuchoma nyavu hizo, hapo kweli ana nia ya kuwakomboa
watanzania hususani wakulima na wafugaji,” alihoji Lembeli.
0 maoni:
Chapisha Maoni