Baada ya kung’ara katika mchezo wa kwanza wa kujiandaa na msimu mpya wa ligi nchini England pamoja na barani ulaya, mshambuliaji Chuba Akpom amejitengenezea mazingira ya kubaki katika kikosi cha kwanza cha Arsenal, kufuatia uhakika uliotangazwa na meneja wa klabu hiyo ya jijini London, Arsene Wenger.
Akpom, aliifungia Arsenal mabao matatu kati ya manne yaliyoipa ushindi The Gunnes katika mpambano wa Beckleys Asia Trophy, dhidi ya kikosi Singapore Best 11 hapo jana huku bao lingine likifungwa na kiungo Jack Wilshere.
Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger alipozungumza na waandishi wa habari mara baada ya mtanange huo uliounguruma nchini Singapore alikiri kuridhishwa na kiwango cha mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 19.
Wenger, amesema anaamini Akpom amekomaa kwa sasa, baada ya kumtoa kwa mkopo mara kadhaa, hivyo hana budi kumpa nafasi katika kikosi chake kuanzia msimu ujao wa ligi.
Mzee huyo wa kifaransa amesema amefarijika kuona kazi kubwa ikifanywa na mshambuliaji huyo ambaye ni mzaliwa wa nchini Ghana, kwa kuisaidia timu hasa katika mchezo wa jana ambao ulionekana kuwa na upinzani mkubwa kutoka kwa wenyeji wao.
Ushindi wa Arsenal katika mchezo wa jana, umewapeleka katika hatua ya fainali ya michuano ya Backleys Asia Trophy ambao utawakutanisha na Everton kutoka nchini England.
Everton walifanikiwa kutinga katika hatua ya fainali baada ya kuifunga Stoke City kwa changamoto ya mikwaju ya penati nne kwa tano.
Mchezo huo wa fainali umepangwa kufanyika siku ya jumamosi.
0 maoni:
Chapisha Maoni