Baadhi
ya viongozi wa chama cha mapinduzi waliohamia chama cha demokrasia na
maendeleo Chadema mkoa wa Kilimanjaro wamesema wameanza kupokea vitisho
vya kuhatarisha usalama wa maisha yao ikiwemo kutekwa na kuteswa.
Hayo yamebainishwa na aliyekuwa mwenyekiti wa umoja wa vijana wa
chama cha mapinduzi mkoa wa Kilimanjaro Bw.Fredy Mushi na aliyekuwa
katibu wa fedha na uchumi CCM mkoa wa Kilimanjaro Bw.Paul Matemu wakati
wakikabidhiwa kadi za baraza la vijana wa chama cha demokrasia na
maendeleo katika manispaa ya Moshi.
Wamesema pamoja na vitisho ambavyo wameanza kupokea hawataogopa na
kwamba wamejiandaa ipasavyo kufanya kampeni za kistaarabu ili
kuhakikisha wanapata viongozi bora wenye sifa na kufikia lengo la kuleta
mabadiliko ya kweli kupitia vyama vinavyounda umoja wa katiba ya
wananchi(UKAWA).
Mapema akikabidhi kadi kwa wananchama hao mwenyekiti wa baraza la
vijana wa chama cha demokrasia na maendeleo (Chadema)katika manispaa ya
Moshi Bw.Dominick Tarimo amewataka vijana kujitokeza kwa wingi kupiga
kura na kuahidi kufanya kampeni za kistarabu bila vurugu ili kuhakikisha
uchaguzi ambao unatarajia kufanyika Oktoba 25 mwaka huu unamalizika kwa
amani na utulivu.
Naye katibu wa baraza la vijana Chadema Bw.Deogratius Kiwelu
amewataka viongozi wanaotoka chama cha mapinduzi na kujiunga na chama
hicho kufuata sheria na kanuni za chama hicho ili kupata ushindi wa
kishindo kuanzia ngazi ya uraisi, wabunge na madiwani.
0 maoni:
Chapisha Maoni