Madiwani
18 wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro kupitia Chama Cha Mapinduzi
(CCM) wametangaza kuhama chama hicho jana jijini Arusha.
Madiwani hao waliotangaza kuihama CCM walikuwa katika ofisi za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wilayani Arumeru.
Huku
aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Elias Ngorisa aliyefuatana na
Diwani wa Kata ya Engusero Sambu, Kagil Mashati Ngukwo, ambaye pia
alikuwa Katibu wa Fedha na Uchumi wa CCM Wilaya ya Ngorongoro naye pia
amejiunga na Chadema.
Walikuwepo
wazee wa mila wa Kabila la Wamasai (malaigwanani) Laurence Ngorisa na
Lekakui Oleiti, wote kutoka Engusero Sambu. Mbunge wa Arumeru Mashariki,
Joshua Nassari, ndiye aliyewapokea makada hao na kuwapatia kadi za
Chadema.
Akizungumza
baada ya kupokea kadi, Elias Ngorisa, alisema wapo madiwani 18 kati ya
28 ambao tayari wamechukua kadi za Chadema na kuondoka CCM na watatetea
nafasi zao kupitia Chadema katika uchaguzi wa Oktoba mwaka huu.
Alisema
yapo mabadiliko makubwa na Watanzania hawana budi kuyakubali na
ameshawishika kubadilisha mwelekeo toka CCM kwenda Chadema.
Kwa
upande wake, Diwani Ngukwo, alisema, amekihama chama hicho kwa sababu
anahitaji mabadiliko na anaamini wengi watawafuata ili waweze kuondokana
na manyanyaso mengi ya Loliondo wanayopata.
0 maoni:
Chapisha Maoni