Mshambulizi wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta amesema
amesalia na nafasi moja tu ya kucheza Klabu bingwa ya dunia. Akizungumza
na mwandishi wa mtandao huu ( Baraka Mbolembole) Jumanne hii, Samatta
ambaye amebakiza miezi 8 katika mkataba wake wa sasa.
Samatta ataachana na TP Mazembe ya DR Congo klabu ambayo alijiunga
nayo Mei, 2011 akitokea Simba SC. " Nimebakiwa na nafasi moja tu, nayo
ni ushiriki wa TP katika ligi ya mabingwa msimu huu ambako tuko robo
fainali. Kama timu itafanya vizuri, naweza kucheza michuano ya Klabu
bingwa ya dunia"
Samatta amedhamiria kuachana na TP ambayo tangu amejiunga nayo
ameshuhudia wachezaji wasiozidi saba wakiuzwa nje au ndani ya bara la
Afrika. Mazembe tayari imecheza michezo miwili katika hatua ya makundi
ya ligi ya mabingwa lakini haijapata ushindi wowote na wamecheza mechi
zote hizo pasipo kufunga goli lolote.
" Nimeshiriki karibu dakika 120 katika michezo miwili ambayo
tumecheza katika nane bora. Suala la kupata goli/magoli ni kutokana na
upinzani tunaokutana nao. Kitu kizuri pia, hatujaruhusu goli. Kwa hiyo
unaweza kuona upinzani jinsi ulivyo" anasema Samatta na kuongeza
" Tangu nimejiunga hapa ni wachezaji wasiozidi Saba wameuzwa. Ukweli
sijafanya mawasiliano na mchezaji yeyote ambaye alikuwa akichezea TP.
Nahitaji changamoto mpya. Wakala wangu bado anashughurika na hilo.
Dirisha la usajili liko wazi hivyo lolote linaweza kutokea "
Habari za ndani ambazo pia ninazo ni kwamba, mchezaji huyo wa timu ya
taifa ya Tanzania, Taifa Stars anaweza kuwa mchezaji anayelipwa zaidi
barani Afrika kama hatokwenda barani ulaya mara baada ya kumalizika
mkataba wake wa sasa. Samatta aliondoka Tanzania akiwa na miaka 19. "
Nafasi ya kusaini mkataba mpya hapa ni ndogo sana" anamaliza kusema
mchezaji huyo mwenye miaka 23 hivi sasa
0 maoni:
Chapisha Maoni