Katika
hali isiyokuwa ya kawaida, baadhi ya wanachama wa chama cha mapinduzi
kata ya Bugogwa wilayani Ilemela, leo asubuhi wamevamia katika ofisi za
wilaya hiyo na kumshabulia kwa kipigo katibu wa chama hicho wilayani
humo Bw. Acheni Maulid wakipinga kukatwa kwa jina la mgombea aliyeshinda
kwenye kura za maoni kwa madai kuwa ni mkimbizi.
Tukio hilo limetokea majira ya saa 5 asubuhi baada ya wanachama hao
kuwasili katika ofisi za CCM wilayani humo zilizopo eneo la maliasili
pasiansi, kwa lengo la kutaka kufahamu sababu za Maliki Hatibu kukatwa
jina lake na kudaiwa kuwa si raia wa Tanzania licha ya kushinda kwa kura
720 dhidi ya kura 597 alizopata mshindi wa pili Steven Mashamba kwenye
kura za maoni zilizofanyika Agosti mosi mwaka huu.
Askari polisi wakiwa na silaha na mabomu ya machozi walilazimika
kuimarisha ulinzi katika eneo lote linalozunguka ofisi za chama hicho,
huku baadhi ya wanachama wakichana kadi zao na wengine kwa hasira
wakivua nguo na kubakia uchi huku wakijiapiza kuwa kamwe hawataondoka
katika eneo hilo bila jina la Maliki Hatibu.
Katibu wa CCM wilayani Ilemela Acheni Maulid amezungumza na
waandishi wa habari ofisini kwake na kutoa ufafanuzi kuhusu tuhuma
zinazoelekezwa kwa mshindi huyo wa kura za maoni, ambapo ITV
imewasiliana kwa njia ya simu na mgombea huyo Maliki Hatibu kwa lengo la
kutaka kufahamu ukweli kuhusu uraia wake.
SOURCE: ITV
0 maoni:
Chapisha Maoni